SEHEMU YA NNE
Kazi Mbalimbali Katika Maeneo ya Vijijini
Ardhi Itupatie Mahitaji Yetu
Kwa mibaraka yake Mungu, ardhi hii ikilimwa itatupatia mahitaji yetu. Tusikate tamaa kwa mambo ya maisha haya kwa sababu ya kuonekana hali ile ya kushindwa, wala tusivunjike moyo kwa kuchelewa mambo. Yatupasa kuulima udongo kwa furaha, matumaini, na shukrani, tukisadiki ya kwamba ndani ya udongo huo kuna hazina nyingi za kuweka ghalani mwetu kwa mfanyakazi mwaminifu, yaani, hazina zile zenye utajiri mwingi kuliko dhahabu na fedha. Shutuma ile inayotolewa kwake [huo udongo] kuwa ni mnyimivu [hautupatii mavuno ya kutosha] ni ya uongo. Kwa kuilima vizuri na kutumia akili ardhi itatoa hazina zake [mazao] kwa manufaa ya mwanadamu. Milima na vilima hubadilika; dunia huchakaa kama vazi kuukuu; lakini mbaraka wa Mungu, unaoandaa meza [chakula] jangwani kwa ajili ya watu wake, hautakoma kamwe.
Nyakati ngumu sana zi mbele yetu, tena ipo haja kubwa kwa familia kutoka mijini kwenda kule shamba [vijijini], kweli yaweza kupelekwa katika vichochoro sawasawa tu na vile inavyoweza kupelekwa katika njia kuu za usafiri za dunia hii. Mengi hutegemea juu ya kupanga mipango yetu kulingana na Neno la Bwana, na kwa juhudi ya kudumu kuitekeleza [mipango hiyo]. Mambo mengi sana hutegemea bidii yetu iliyotolewa wakf pamoja na ustahimilivu wetu kuliko kutegemea akili nyingi isiyo ya kawaida na maarifa yale yapatikanayo katika vitabu ambayo hayatendewi kazi. Talanta zote na uwezo wote aliowapa mawakala wake wa kibinadamu, visipotumika, basi, havina faida yo yote kwetu.
Kuzirudia njia zile rahisi [za utendaji kazi] kutathaminiwa na watoto na vijana wetu. Kazi ya bustanini na shambani italeta badiliko linalokubalika badala ya kawaida zile zinazochosha sana za masomo ya kinadharia, ambayo akili za watoto wao wadogo zisingejihusisha nayo kwa muda mrefu. Kwa mtoto mdogo aliye dhaifu kiakili, ambaye anaona masomo ya vitabuni kuwa yanamchosha sana, na kwake huwa ni vigumu kuyakumbuka, kazi kama hiyo itakuwa na manufaa ya pekee kwake. Kuna afya na furaha kwa ajili yake katika kujifunza maumbile [viumbe vya asili]; na picha inayozama moyoni mwake haitaweza kufifia, kwa maana mambo hayo yatahusishwa na vitu vile vilivyo mbele ya macho yake daima. ----- Testimonies, Gombo la 6, uk. 178,179. (1900)
Mkiwa na Kipande Kidogo cha Ardhi na Nyumba Nzuri ya Kuishi
Ardhi inapaswa kushughulikiwa mpaka iweze kutoa nguvu yake; lakini pasipo kuwapo mbaraka wa Mungu haiwezi kutoa kitu. Hapo mwanzo, Mungu aliangalia vyote alivyoviumba, na kusema kwamba vilikuwa vyema sana. Laana ililetwa juu ya nchi [udongo] kama matokeo ya dhambi. Lakini, je! laana hiyo izidi kuongezeka kwa kuzidi kufanya dhambi? Ujinga unaendelea kuleta matokeo yake yanayoleta madhara mengi. Watumishi walegevu [wavivu] wanazidisha maovu kwa tabia zao za kivivu. Wengi hawako tayari kujipatia chakula chao kwa jasho la uso wao, wanakataa kuilima ardhi. Lakini ardhi inazo hazina zake zilizojificha chini kwa ajili ya wale walio na ujasiri na nia na uvumilivu wa kuzikusanya hazina zake hizo. Akina baba na mama walio na kipande cha ardhi na nyumba nzuri ya kuishi, hao ni wafalme na malkia.
Wakulima wengi wameshindwa kupata mavuno ya kutosha kutoka katika mashamba yao kwa sababu wameichukulia kazi hiyo kana kwamba ni kazi ya kudhalilisha mno; hawatambui kwamba kuna mbaraka ndani yake kwa ajili yao wenyewe na familia zao. Yale yote wanayofahamu wao ni kwamba kazi hiyo ni utumwa wa aina fulani. Mashamba yao ya miti izaayo matunda huachwa bila kutunzwa, mazao hayapandwi kwa majira yake yanayofaa, na kazi ya juu juu tu hufanywa katika kuilima ardhi hiyo. ----- Fundamentals of Christian Education, uk. 326,327. (1894)
Matunda, Mboga za Majani, na Kuku Vyapendekezwa kwa Eneo Moja
Katika ujirani huu kuna eneo kubwa la ardhi isiyokaliwa na watu. Baadhi ya watu wetu wanaoishi katika mazingira ya hali ya hewa iliyosumishwa huko mijini wangeweza kunufaika kwa kujipatia ekari chache za ardhi hii. Wangeweza kujipatia mahitaji yao ya maisha kwa kupanda matunda na mboga za majani na kufuga kuku. Hospitali yetu ingefurahi kununua mayai na mboga za majani kutoka kwao. Natamani kwamba mradi fulani kama huo ungeanzishwa hapa. Baraka kubwa ingewajia wazazi hao pamoja na watoto wao, endapo wangeondoka katika miji hiyo miovu, iliyochafuliwa na kwenda katika sehemu zile za shamba [vijijini]. ----- Letter 63, 1904.
Kuishi Mashambani [Vijijini] - Mbaraka Kwa Maskini
Endapo maskini ambao hivi sasa wamesongamana mijini wangepata makazi yao huko mashambani [vijijini], wasingeweza kujipatia riziki yao tu, bali wangepata afya na furaha ambayo mpaka sasa hawaijui. Mara nyingi [huko mijini] kazi ngumu, chakula duni, na kubana mno matumizi, shida na umaskini, hiyo ndiyo ingekuwa sehemu ya maisha yao. Lakini ni mbaraka ulioje ambao ungekuwa wao kama wangeondoka mjini, na kuviachilia mbali vishawishi vyake vinavyowaelekeza watu maovuni, kuachana na machafuko yake na uhalifu, huzuni na uchafu wake, na kwenda mashambani [vijijini] kwenye utulivu na amani na usafi.
Kwa wengi miongoni mwa wale wanaoishi mijini ambao hawana hata kipande kidogo cha majani mabichi cha kuweza kuweka miguu yao juu yake, ambao mwaka nenda mwaka rudi wameziangalia nyua zao zilizojaa uchafu na njia zile finyu za vichochoroni, kuta zile za matofali ya kuchoma na sakafu za mawe za kutembea juu yake, mbingu zile zilizojaa vumbi na moshi, ----- kama hao wangepelekwa kwenye wilaya moja yenye mashamba ya kulima, yaliyozungukwa na mashamba ya chanikiwiti, misitu midogo, na vilima na vijito, mbingu safi na zenye hewa safi, na hewa safi ile ya mashambani, basi, kwao hao ingekuwa karibu sawa na [kuishi] mbinguni.
Mawasiliano yao yakiwa yamekatwa kwa kiwango kikubwa hata wasiweze kuonana na watu wengine wala kuwategemea, tena wakiwa wametengwa mbali na semi zile chafu za ulimwengu pamoja na desturi zake na misisimko yake, wangeweza kukaribia sana kwenye maana ya ndani kabisa ya maumbile. Kuwako kwake Mungu kungesikika na kuwa dhahiri sana kwao. Wengi wangejifunza kwake fundisho lile la kumtegemea yeye. Kupitia katika maumbile hayo wangeweza kuisikia sauti yake mioyoni mwao ikiwatamkia amani na upendo wake, na akili na roho na mwili wao vingeweza kuitikia uponyaji huo, ulio na uwezo wa kuwapa uzima. ----- The Ministry of Healing, uk. 190-192. (1905).
Viwanda Vidogo Mbalimbali Kwa Familia Zitokazo Mijini
Waumini wale ambao kwa sasa wanaishi mijini inawapasa kwenda shamba [vijijini], ili wapate kuwaokoa watoto wao na maangamizi. Mawazo yanapaswa kuelekezwa upande wa kuanzisha viwanda [vidogo] ambamo familia hizo zinaweza kupata kazi. Wale wanaosimamia kazi ya Shule na wangeona kile kinachoweza kufanywa na taasisi hizo zingeweza kuanzisha viwanda [vidogo] kama hivyo, ili watu wetu wanaotaka kuondoka mijini, waweze kujipatia makazi yao yanayofaa bila kutumia fedha nyingi sana, na pia kuweza kupata kazi huko. Katika sehemu zote mbili na kuna hali nzuri ya ardhi ambayo inatia moyo kuweza kuuendeleza mpango kama huo. Jifunzeni hali ya nchi ilivyo.
Yale yote yanayotakiwa kufanywa hayawezi kuelezwa kinagaubaga mpaka hapo mwanzo utakapofanywa. Liombeeni jambo hilo, tena kumbukeni kwamba Mungu ameshika usukani, kwamba yeye ndiye anayeongoza katika shughuli zote za kibiashara. Mahali pale kazi inapoendeshwa kwa njia inayotakiwa panakuwa fundisho la mfano linalopaswa kuigwa na mahali pengine [patakapofunguliwa]. Pasiwe na ufinyu wo wote [wa mawazo], wala ubinafsi, katika kazi hiyo inayofanyika mahali hapo. Kazi hiyo inatakiwa kuwekwa juu ya msingi rahisi, unaoweza kutekelezwa. Wote hawana budi kufundishwa ya kuwa sio tu kukiri kwamba wanaiamini kweli, kama vile kweli yenyewe ilivyo, bali kuionyesha kweli hiyo kwa mfano katika maisha yao ya kila siku. ----- Letter 25, 1902.
Kazi ya Kuuza Chakula Kiletacho Afya
Shughuli [biashara] hiyo ya [kuuza] chakula kiletacho afya inapaswa kuanzishwa hapa [Avondale]. Hiyo ingekuwa mojawapo ya viwanda vinavyohusiana na Shule. Mungu ameniagiza mimi kwamba wazazi wanaweza kupata kazi katika kiwanda hicho, na kuwapeleka watoto wao shuleni. Lakini kila kitu kinachofanyika hapo kinapaswa kufanywa kwa njia iliyo rahisi sana. Pasiwepo na ubadhirifu [matumizi mabaya] wo wote katika jambo lo lote lile. Kazi thabiti inapaswa kufanywa, kwa sababu kazi isipofanywa kwa uthabiti, matokeo yake yatakuwa kazi ya ovyo ovyo tu. ----- Australasian Union Conference Record, Julai 28, 1899.