SEHEMU YA KWANZA
Wito wa Kuihama Miji
Hatari Kubwa Zilizomo Mijini
Ni wachache wanaotambua umuhimu wa kukwepa, kwa kadiri iwezekanavyo, uhusiano wo wote ule unaoleta uadui kwa maisha yetu ya kidini. Katika kuchagua mazingira yao, ni wachache mno wanaoweka mawazoni mwao ufanisi wao wa kiroho katika nafasi ya kwanza.
Wazazi na familia zao hukimbilia mijini, kwa sababu wanadhani kwamba ni rahisi kupata maisha mazuri huko kuliko mashambani [vijijini]. Watoto wao, wakiwa hawana kazi yo yote ya kufanya wasipokuwa shuleni kwao, hujipatia elimu ya mitaani. Kutoka kwa marafiki zao waovu wanajifunza tabia za uovu na ubadhirifu [utumiaji mbaya wa fedha na vitu]. Wazazi huyaona hayo yote, lakini itahitaji kujitolea mhanga kuweza kuyasahihisha makosa yao hayo, nao [wazazi] huendelea kuishi mahali hapo walipo mpaka Shetani anawatawala watoto wao kabisa.
Ni afadhali kujinyima mambo yote na kila tarajio la kidunia kuliko kuzihatirisha roho hizo za thamani mlizokabidhiwa kuzitunza. Watashambuliwa vikali na majaribu, nao yapasa wafundishwe jinsi ya kuyakabili; lakini ni wajibu wenu kuuondolea mbali kila mvuto, kulivunjilia mbali kila zoea, kukata kila kifungo kinachowazuia msiwe na uhuru kamili, ulio wazi, na kujitoa wakf ninyi wenyewe kwa moyo wenu wote pamoja na familia yenu kwa Mungu.
Badala ya msongamano wa watu uliomo mjini, tafuteni mahali fulani palipo kimya [pa upweke] kwa kadiri iwezekanavyo, mahali palipo salama mbali na majaribu, nanyi mkiwa pale waleeni na kuwaelimisha ili wapate kuwa watu wenye manufaa katika maisha yao. Nabii Ezekieli ndivyo anavyoorodhesha sababu zilizoifanya Sodoma kutenda dhambi na kuangamizwa: "Kiburi, chakula tele, na uvivu mwingi vilikuwa ndani yake pamoja na binti zake [vitongoji vyake]; wala haukuitia nguvu mikono ya maskini na wahitaji." Wale wote wanaotaka kuokoka ili wasipatikane na maangamizi kama yale ya Sodoma, hawana budi kuukwepa mwenendo ule ulioleta hukumu za Mungu juu ya mji ule mwovu." ----- Testimonies, Gombo la 5, uk. 232,233 (1882).
Kuishi Mijini Sio Mpango wa Mungu
Ulimwenguni kote miji inageuka na kuwa mahali penye maovu mengi sana. Kila upande huonekana mambo machafu na sauti za uovu. Kila mahali kuna vishawishi vya kuamsha ashiki [tamaa mbaya ya uasherati] na ubadhirifu [matumizi mabaya ya mali na vitu]. Wimbi la rushwa na uhalifu linazidi kuumuka daima. Kila siku inayopita huleta taarifa za kutumia nguvu ----- ujambazi, mauaji, kujiua, na uhalifu mwingine usiostahili hata kutajwa.
Maisha yaliyomo mijini sio maisha halisi, tena ni ya kinafiki. Tamaa kubwa sana ya kupata fedha, mambo ya mpwitompwito [msisimko] yapitayo kasi pamoja na kutafuta anasa, kiu ya kuwakoga [kujionyesha ufahari kwa] wengine, utajiri na ubadhirifu, mambo yote hayo ni nguvu ambazo, kwa sehemu kubwa sana ya wanadamu, huyageuzia mawazo yao mbali na kusudi halisi la maisha yao. Wanaufungua mlango wa kuingiza ndani yao maelfu ya maovu. Kwa vijana mambo hayo yana nguvu nyingi ambayo karibu haizuiliki kabisa.
Mojawapo ya majaribu yaliyojificha sana na ya hatari sana yanayowashambulia mno watoto na vijana katika miji ni kule kupenda anasa [starehe]. Sikukuu ni nyingi; michezo na mashindano ya mbio za farasi huwavuta maelfu, na ule mpwitompwito upitao upesi pamoja na anasa huwavuta kwenda mbali na majukumu mazito ya maisha yao. Fedha ambayo ingetunzwa kwa ajili ya kuitumia kwa mambo mazuri zaidi hutapanywa ovyo katika burudani zao nyingi.
Kutokana na utendaji wa mashirika ya amana, na matokeo ya vyama vya wafanya kazi na migomo yake, hali ya maisha mjini daima inakuwa ngumu zaidi na zaidi. Taabu kubwa ziko mbele yetu; na kwa familia nyingi kuondoka kwao kutoka mijini kutakuwa ni kwa lazima.
Mazingira ya nje katika miji mara nyingi ni ya hatari kubwa kwa afya. Uwezekano wa kudumu wa kupatwa na magonjwa, kuenea kwa hewa chafu, maji machafu, chakula kilichochafuliwa, majengo yaliyosongamana pamoja yenye giza na yasiyofaa kiafya, ni baadhi ya mambo mabaya ya kukabiliana nayo humo.
Halikuwa kusudi la Mungu kwamba watu waishi kwa kusongamana sana mijini, wakisongamana pamoja katika mlolongo wa majumba katika kitalu kimoja na katika nyumba za kupangisha zenye vyumba vingi. Hapo mwanzo aliwaweka wazazi wetu wale wa kwanza katikati ya madhari nzuri na sauti nzuri. Anataka sisi tuifurahie siku ya leo. Kadiri tunavyokaribia sana kuwa katika hali ile inayopatana na mpango wa Mungu wa awali, ndivyo kadiri tutakavyokuaa na nafasi nzuri zaidi ya kujipatia afya ya mwili, akili, na roho. ----- The Ministry of Healing, uk. 363-365. (1905)
Moyo wa Kusitasita
Sikuweza kulala baada ya kupita saa nane ya usiku mpaka asubuhi ya leo. Wakati wa usiku nilikuwa natoa ushauri. Nilikuwa nazisihi baadhi ya familia kutumia njia alizoziweka Mungu, na kuondoka mijini ili kuwaokoa watoto wao. Wengine walikuwa wanasitasita tu, bila kufanya juhudi yo yote iliyo dhahiri.
Malaika wale wenye rehema walimharakisha Lutu na mkewe na binti zao kwa kuwashika mikono yao. Lutu angekuwa ameharakisha kama Mungu alivyotaka, mke wake asingegeuka na kuwa nguzo ya chumvi. Lutu alikuwa na roho hiyo ya kuchelewa-chelewa [kusitasita] mno. Hebu sisi na tusiwe kama yeye. Sauti ile ile iliyomwonya Lutu kuondoka Sodoma inatuamuru sisi, ikisema, "Tokeni kati yao, mkatengwe nao... Msiguse kitu kilicho kichafu." [2 Kor. 6:17.] Wale wanaolitii onyo hilo watapata kimbilio. Hebu kila mwanaume na awe macho sana kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, tena ajaribu kuiokoa familia yake. Hebu na ajifunge kibwebwe [mkanda] kwa kazi hiyo. Mungu ataonyesha hatua kwa hatua linalopaswa kufanywa baada ya hapo.
Isikilizeni sauti ya Mungu kupitia kwa mtume wake Paulo, isemayo: "Utimizeni wokovu wenu kwa kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema" [Wafilipi 2:12,13]. Lutu akalikanyaga bonde lile tambarare kwa hatua za kujilazimisha na kuchelewa-chelewa tu. Kwa muda mrefu sana alikuwa amezoeana na watenda maovu wale hata hakuweza kuiona hatari kubwa iliyomkabili mpaka hapo mke wake aliposimama katika bonde lile akiwa nguzo ya chumvi milele." ----- Review and Herald, Des. 11, 1900.
Miji Itapatilizwa kwa Hukumu za Mungu
Wakati umekaribia ambapo miji mikubwa itapatilizwa kwa hukumu za Mungu. Katika kitambo kidogo tu kilichobaki, miji hiyo itatikiswa vibaya mno. Haidhuru iwe mikubwa kiasi gani au majengo yake yawe imara jinsi gani, haidhuru vifaa vya kujihami na moto viwe vimeandaliwa kwa wingi namna gani, acha Mungu ayaguse majengo hayo, katika muda wa dakika chache tu au saa chache yatakuwa yameharibiwa kabisa na kuwa magofu.
Miji hiyo miovu [isiyomcha Mungu] itafagiliwa mbali kwa fagio la maangamizi. Katika uharibifu unaoyapata majengo makubwa na sehemu kubwa za miji hivi sasa, Mungu anatuonyesha kile kitakachoiangukia dunia yote. ----- Testimonies, Gombo la 7, uk. 82,83. (1902).
Matokeo ya Maonyo Yaliyopuuzwa
Nimeagizwa kutangaza ujumbe huu kuwa miji ile iliyojaa maasi [uvunjaji wa sheria], na ile iliyo miovu kupita kiasi, itaharibiwa kwa matetemeko, kwa moto, na kwa mafuriko. Dunia yote itaonywa na kujua kwamba yuko Mungu atakayedhihirisha mamlaka yake kama Mungu. Mawakala [wajumbe] wake wasioonekana kwa macho [malaika] watasababisha maangamizi, kuteketeza kwa moto, na vifo. Utajiri wote uliolundikwa utakuwa kama si kitu....
Maafa yatakuja ----- yaani, maafa ya kuogofya mno, yasiyotarajiwa kabisa; na maangamizi hayo yatafuatana moja baada ya jingine. Kama watu watayasikia [watayatendea kazi] maonyo haya ambayo Mungu ametoa, na iwapo makanisa yatatubu, na kurudia utii wao [kwa Mungu], basi, miji mingine itaachwa isiharibiwe kwa muda fulani. Lakini endapo watu waliodanganyika wataendelea kutembea katika njia ile ile walimokuwa wakitembea, wakiendelea kuidharau Sheria ya Mungu [Amri Kumi], na kuhubiri [mafundisho ya] uongo mbele ya watu, basi, Mungu ataruhusu majanga yawapate ili akili zao zipate kuamshwa.
Bwana hatawatupilia mbali kwa ghafula wale wote wanaozivunja amri zake [kumi], wala kuyaangamiza mataifa mazima; lakini ataiadhibu miji na mahali pale ambapo watu wamejitoa kabisa kutawaliwa na nguvu za kishetani. Kwa ukali sana miji ya mataifa itashughulikiwa, hata hivyo haitapatilizwa kwa ghadhabu kali mno ya Mungu, kwa sababu baadhi ya watu waliomo humo watajinasua kutoka katika madanganyo hayo ya yule adui [Shetani], kisha watatubu na kuongolewa, na wakati uo huo watu wengi sana watakuwa wanajiwekea akiba ya ghadhabu kwa siku ile ya ghadhabu [ya Mwana-Kondoo, yaani, Kristo]. [Ufunuo 6:14-17; 15:1; 16:1-21.] ----- Evangelism, uk. 27. (1906)
Ukaribu Sana wa Kuja kwa Hukumu za Mungu
Zipo sababu kwa nini sisi tusijenge [nyumba zetu] mijini. Juu ya miji hii, hukumu za Mungu zi karibu sana kuiangukia. ----- Letter 158, 1902.
Laiti kama watu wa Mungu wangeyajua maangamizi yaliyo karibu sana kuja juu ya maelfu ya miji, ambayo kwa sasa imejisalimisha kabisa kuabudu sanamu [Kol. 3:5,6; Efe. 5:5-7; Kut. 20:4-6]. ----- Review and Herald, Sept. 10, 1903.
Maono ya Maangamizi Makubwa
Alfajiri Ijumaa iliyopita, kabla tu sijaamka usingizini, mandhari [picha] iliyonigusa sana moyoni ilionyeshwa mbele yangu. Nikajiona kana kwamba nimeamka usingizini, ila sikuwa nyumbani mwangu. Kupitia katika madirisha niliweza kuona moto mkubwa wa kutisha uliokuwa unayateketeza majumba. Mipira mikubwa ya moto [huenda ikawa ni mabomu] ilikuwa ikidondoka juu ya nyumba zile, na kutoka katika mipira hiyo mishale ya moto ilikuwa inaruka kuelekea kila upande. Ilikuwa haiwezekani kabisa kuizuia mioto hiyo iliyokuwa imewashwa, tena mahali pengi palikuwa panaharibiwa. Hofu kuu iliyowashika watu ilikuwa haielezeki. ----- Evangelism, uk. 29. (1900)
Juhudi za Mungu za Kuwaamsha Watu
Nikiwa bado ningali pale Loma Linda, California, Aprili 16, 1906, maono ya ajabu sana yalipita mbele yangu. Wakati wa njozi zangu za usiku, nalikuwa nimesimama kwenye mwinuko [kilima], kutoka hapo niliweza kuziona nyumba zikitikiswa kama tete katika upepo. Majengo, makubwa kwa madogo, yalikuwa yakianguka chini. Majumba ya anasa wanayoyatembelea watu wengi, nyumba za michezo ya kuigiza, hoteli, na nyumba za matajiri zilitikiswa na kuharibiwa kabisa. Maisha mengi yakafutiliwa mbali, na anga ilikuwa imejaa sauti za vilio vikubwa kutokana na wale waliokuwa wamejeruhiwa na kuogofywa sana.
Malaika wa Mungu waangamizao walikuwa wanafanya kazi yao. Mguso mmoja tu, majengo yaliyojengwa imara sana ambayo watu walifikiri kwamba yalikuwa salama kutokana na hatari ya kila namna, kwa ghafula yakawa malundo ya takataka. Hapakuwa na hakika ya kuwa na usalama mahali po pote pale. Mimi sikujiona kuwa nimo katika hatari yo yote maalum, lakini utisho mkuu wa matukio yale yaliyopita mbele yangu mimi siwezi kupata maneno ya kuelezea. Ilionekana kana kwamba uvumilivu wa Mungu ulikuwa umefikia kikomo chake kabisa, na ya kwamba siku ile ya hukumu ilikuwa imekuja.
Malaika yule aliyekuwa amesimama kando yangu ndipo akanipasha habari kwamba ni wachache tu waliokuwa na wazo lo lote kuhusu uovu uliomo katika ulimwengu wetu hivi leo, na hasa uovu ule ulio katika miji mikubwa. Akatangaza kwamba utawala wa Mungu ulio mkuu kuliko wote, na utakatifu wa Sheria yake [Amri Kumi], havina budi kufunuliwa kwa wale wanaoendelea kukataa kutoa utii wao kwa Mfalme huyo wa wafalme. Wale wanaochagua kubaki katika hali yao ya uasi [kuvunja Amri zake Kumi], ni lazima wapatilizwe kwa hukumu kwa rehema [zake Mungu], ili, kama ikiwezekana, wapate kuamshwa [kuzinduliwa] watambue uovu wa njia yao. ----- Testimonies, Gombo la 9, uk. 92,93. (1909)
Hatari Itakayowakabili Watakaoendelea Kubaki Mjini Bila Sababu
Kulingana na nuru ile niliyopewa, mimi nawasihi watu kutoka na kuvihama vituo vikubwa vilivyojaa watu wengi. Miji yetu inazidi kuwa miovu, tena, inaonekana wazi zaidi na zaidi ya kwamba wale watakaobaki ndani ya miji hiyo bila sababu [ulazima wo wote] watafanya hivyo kwa athari kubwa ya wokovu wa nafsi zao. ----- Manuscript 115, 1907.