HIVI KRISTO NI KIUMBE KILICHOUMBWA?
Kabla hatujapita na kwenda kwenye masomo mengine yenye manufaa katika maisha yetu, ambayo yanapaswa kujifunzwa kutokana na kweli hizi, tutatumia muda mfupi juu ya wazo ambalo kwa uaminifu linashikwa na wengi, ambao kwa dhana yo yote ile wasingeweza kumvunjia heshima Kristo kwa makusudi, lakini ambao, kupitia kwa wazo hilo wanaukana kabisa Uungu wake. Wazo hilo ni kwamba Kristo ni kiumbe kilichoumbwa ambaye kwa mapenzi yake Mungu alipandishwa cheo kufikia cheo cha juu alicho nacho sasa. Hakuna ye yote mwenye mtazamo huu awezaye kuwa na picha sahihi ya cheo halisi cha Kristo anachokalia hivi sasa.
Mtazamo huu katika hoja hii umejengwa juu ya kutoelewa vyema fungu moja, Ufu.3:l4: "Na kwa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo Yeye aliye Amina, Mwanzo wa kuumba kwa Mungu." Fungu hili hutafsiriwa kwa makosa kumaanisha kwamba Kristo ndiye kiumbe cha kwanza alichokiumba Mungu; kwamba kazi ya Mungu ya uumbaji ilianzia kwa Yeye (Kristo). Lakini mtazamo huu unapingana na Maandiko yasemayo kwamba Kristo Mwenyewe ndiye aliyeviumba vitu vyote. Kusema kwamba Mungu alianza kazi yake ya uumbaji kwa kumuumba Kristo ni kumwondoa kabisa Kristo katika kazi ya uumbaji.
Neno lililotafsiriwa "Mwanzo" ni ARCHE, likiwa na maana ya "kichwa" au "kuu". Asili yake ni katika jina la Mtawala wa Kiyunani, ARCHON, na hutokea katika "ARCHbishop" (askofu mkuu), na katika "ARCHangel" (malaika mkuu). Angalia Yuda 9; 1 The.4:16; Yohana 5:28,29; Dan.10:21. Hii haina maana kwamba Yeye ni wa kwanza miongoni mwa malaika, kwa kuwa Yeye si malaika, bali yuko juu yao. Ebr.l:4. Ina maana kwamba Yeye ndiye Mkuu au Mfalme wa malaika, kama vile Askofu Mkuu alivyo Mkuu wa Maaskofu. Kristo ni Mkuu (Kamanda) wa Jeshi la malaika. Angalia Ufu. l9:ll-l4. Yeye ndiye aliyewaumba malaika. Kol.1:16. Basi, usemi huu kwamba Yeye ni Mwanzo au Mkuu wa uumbaji wa Mungu, una maana kwamba katika Yeye uumbaji wote ulikuwa na Mwanzo wake; kwamba kama Yeye Mwenyewe asemavyo, Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Ufu. 21:6; 22:13. Yeye ndiye chimbuko vilikotoka vitu vyote.
Wala tusingemfikiria Kristo kama kiumbe, kwa sababu Paulo anamwita Yeye (Kol.1:15) kuwa ni "mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote;" kwa maana mafungu yanayofuata yanamwonyesha Yeye kuwa ndiye Muumbaji, wala siye kiumbe. "Kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika Yeye." Sasa, basi, kama aliumba kila kitu kilichopata kuumbwa,naye alikuwako kabla ya vitu vyote vilivyoumbwa, ni wazi kwamba Yeye Mwenyewe hayumo miongoni mwa vitu vilivyoumbwa. Yeye yuko juu ya viumbe vyote, na sio sehemu yake.
Maandiko yanatangaza kwamba Kristo ni "mzaliwa wa kwanza wa Mungu." Si jukumu letu sisi kupeleleza ni lini alizaliwa, wala akili zetu zisingeweza kuelewa kitu cho chote hata kama tungeambiwa. Nabii Mika anatuambia yale yote tuwezayo kujua juu yake kwa maneno haya, "Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele." Mika 5:2, pambizo. Palikuwa na wakati ambapo Kristo alitoka na kuja kutoka kwa Mungu, kutoka kifuani mwa Baba (Yohana 8:42; 1:l8), lakini wakati huo ulikuwa nyuma sana katika siku zile za milele ambazo kwa akili finyu ya kibinadamu ni kipindi halisi kisichokuwa na mwanzo.
Lakini hoja yenyewe hasa ni kwamba Kristo ni Mwana aliyezaliwa, na sio kiumbe kilichoumbwa. Analo jina tukufu kuliko la malaika alilopata KWA URITHI; Yeye ni "Mwana katika nyumba Yake Mwenyewe." Ebr.1:4; 3:6. Na kwa kuwa Yeye ni Mwana wa Mungu aliye Mzaliwa wa Kwanza, anayo asili moja ile ile na Mungu, na kwa kuzaliwa anazo sifa zote za Mungu ; kwa maana Baba alipendezwa kuwa Mwanawe awe chapa ya nafsi yake, mng'ao wa utukufu wake, akiwa amejazwa na utimilifu wote wa Uungu. Kwa hiyo, anao "uhai ndani yake Mwenyewe;" anayo hali ya kutokufa kama haki yake, naye anaweza kuwapa wengine hali hiyo ya kutokufa. Uhai umo ndani Yake, hakuna awezaye kumwondolea; bali, Yeye Mwenyewe akiutoa kwa hiari yake, anaweza kuutwaa tena. Maneno yake ni haya: "Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa Mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu." Yohana 10:l7,l8.
Kama mtu ye yote analeta ubishano hafifu ule wa zamani, kwamba Kristo angewezaje kuwa na hali ya kutokufa na halafu akafa, sisi tunaloweza kusema tu ni kwamba hatujui. Hatutoi madai yo yote ya kumchimba Mungu. Hatuwezi kuelewa kwa jinsi gani Kristo angeweza kuwa Mungu na wakati uo huo akawa mwanadamu kwa ajili yetu sisi. Hatuwezi kuelewa kwa jinsi gani angeweza kuumba ulimwengu huu kutoka pasipo kitu, wala kwa jinsi gani aliwafufua wafu, wala kwa jinsi gani anafanya kazi yake ndani ya mioyo yetu kwa Roho wake; ila tunaamini hivyo na kuyajua mambo hayo. Yatutosha sisi kusadiki kuwa ni kweli mambo yale aliyoyafunua Mungu, bila kujikwaa kwa mambo yale ambayo hata akili ya malaika haiwezi kuyachunguza. Kwa ajili hiyo, basi, tunafurahia uweza usiokuwa na kikomo na utukufu ambao Maandiko yanatangaza kuwa ni Wake Kristo, bila kuzisumbua akili zetu finyu za kibinadamu kwa kufanya jaribio lisilokuwa na faida yo yote la kueleza vile Mungu alivyo.
Hatimaye, tunaujua umoja wa Mungu Baba na Mwana kutokana na ukweli kwamba wote wanaye Roho yule yule mmoja. Paulo, baada ya kusema kwamba wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu, anaendelea kusema: "Lakini ikiwa Roho wa Mungu, anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake." Rum.8:9. Hapa tunaona kwamba Roho Mtakatifu, pande zote mbili, ni Roho wa Mungu na ni Roho wa Kristo. Kristo "yumo" kifuani mwa Baba;" akiwa kwa asili mwili mmoja na Mungu, naye akiwa na uhai ndani Yake Mwenyewe, kwa halali kabisa anaitwa Yehova, Aliyeko milele, na kama vile aitwavyo katika Yer.23:5,6 ambapo anasemekana kwamba ni Chipukizi la Haki, atakayefanya hukumu na haki katika nchi, atajulikana kwa jina la "YEHOVA-TSIDEKENU" ----BWANA NI HAKI YETU.
Hebu, basi, asiwepo mtu ye yote amheshimuye Kristo, ambaye atampa heshima pungufu kuliko ile anayompa Baba, maana jambo hilo lingekuwa ni kumvunjia heshima Baba kwa kiwango hicho hicho; bali wote, pamoja na malaika mbinguni, na wamsujudu Mwana, pasipokuwa na hofu yo yote kwamba kwa kufanya hivyo wanamsujudu na kumtumikia yule aliye kiumbe badala ya Muumbaji.
Na sasa, wakati jambo hili la Uungu wake Kristo bado limo mioyoni mwetu, hebu na tukae kimya kidogo tukitafakari kisa chake hiki cha ajabu cha kudhalilishwa Kwake.