KWA JINSI GANI TUMTAFAKARI KRISTO ?
Lakini kwa JINSI GANI tungepaswa kumtafakari Kristo? ---- Kwa jinsi ile ile Yeye Mwenyewe alivyojifunua kwa ulimwengu; kulingana na ushuhuda aliotoa unaomhusu Yeye Mwenyewe. Katika hotuba ile ya ajabu iliyoandikwa katika sura ya tano ya Yohana, Yesu alisema: "Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao. Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka." Fungu la 21-23.
Kwake Kristo yametolewa mamlaka ya juu mno, yale ya kuhukumu. Sharti apewe heshima ile ile anayostahili Mungu, naye Neno alikuwa Mungu." Yohana 1:1. Kwamba huyu Neno aliyekuwa Mungu si mwingine ila ni Yesu Kristo tunafunuliwa katika fungu la 14: "Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; (nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba;) amejaa neema na kweli."
Huyo Neno alikuwako "hapo mwanzo." Akili ya mwanadamu haiwezi kuelewa idadi ya miaka iliyofunikwa katika usemi huu. Wanadamu hawajapewa uwezo wa kujua ni lini na ni kwa jinsi gani Mwana alianza kuwa wa pekee; ila tunajua tu kwamba alikuwa Mungu Neno, sio tu kabla ya kuja kwake duniani kutufia, bali pia hata kabla ulimwengu huu haujaumbwa. Muda mfupi tu kabla ya kusulibiwa kwake aliomba hivi: "Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako." Yohana 17:5. Na zaidi ya miaka mia saba kabla ya kuja kwake mara ya kwanza, kuja kwake kulitabiriwa kwa njia ya neno lililovuviwa, likisema: "Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele." Mika 5:2, pambizo (margin). Tunajua kwamba Kristo "alitoka kwa Mungu, naye alikuja" (Yohana 8:42), lakini jambo hilo lilikuwa tangu milele za nyuma sana kiasi cha kupita upeo wa ufahamu wa akili ya kibinadamu.