>Mwanzo >Soma vitabu >Kristo na haki yake >Utangulizi

Utangulizi

Katika fungu  la kwanza la sura ya tatu ya Waebrania tunayapata mausia yanayotolewa kwa Mkristo.  Nayo ni haya: "Kwa hiyo, ndugu watakatifu,wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu."  Kufanya hivyo kama Biblia inavyoagiza, kumtafakari Kristo daima na kwa akili, kama yeye alivyo hasa, kutambadilisha mtu kuwa Mkristo mkamilifu, kwa maana "Kwa kutazama tunabadilishwa."

   Wajumbe wa   Injili wanayo mamlaka iliyovuviwa na Mungu, wanapoliweka neno kuu,Kristo, mbele ya watu kwake peke yake. Paulo alisema kwa Wakorintho, "Maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa." (l Kor.2:2);  tena hakuna sababu yo yote  kudhani kwamba hotuba yake kwa Wakorintho ilikuwa tofauti na hotuba zake alizotoa mahali pengine.  Naam, anatuambia kwamba Mungu alipomdhihirisha Mwanawe kwake, ilikuwa kwamba apate kuwahubiri mataifa (Gal.1:15,16); na furaha yake ilikuwa kwamba  alipewa  neema hii "Kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika." Efe.3:8.

     Lakini ukweli kwamba mitume walimfanya Kristo kuwa mzigo wa  mahubiri yao yote ,huo sio mamlaka yetu ya pekee ya kumtukuza Yeye.  Jina lake ni jina la pekee chini ya mbingu ambalo wanadamu wanaweza kuokolewa kwalo.  Matendo ya Mitume 4:l2.  Yesu mwenyewe alitangaza kwamba hakuna mtu ye yote awezaye  kuja  kwa Baba ila kwa njia Yake.  Yohana l4:6. Kwa Nikodemo alisema, "Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa ; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika Yeye."  Yohana 3:l4,l5.  Huku "kuinuliwa" kwa Yesu, wakati kimsingi hutuelekeza kwenye tendo lile la kusulibiwa kwake, ndani yake kuna mambo mengi zaidi kuliko tukio hilo tu la kihistoria; humaanisha kwamba Kristo hana budi "kuinuliwa" na wale wote wanaomwamini kama Mkombozi  wao aliyesulibiwa, ambaye neema yake na utukufu wake hutosha kukidhi haja kuu kuliko zote ya ulimwengu huu; humaanisha kwamba angepaswa "kuinuliwa juu" katika uzuri wake wote na uweza wake usio na kifani kama "Mungu pamoja nasi," ili kwamba mvuto wake wa ajabu uweze kutuvuta hivyo sisi sote kwake.  Angalia Yohana 12:32.

     Mausia ya kumtafakari Yesu, na pia sababu yake vimetolewa katika Waebrania l2:l-3: "Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na  mwenye kutimiza imani yetu;  ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.  Maana mtafakarini sana yeye aliyestahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka,  mkizimia mioyoni mwenu."  Ni kwa kumtafakari Yesu daima kama alivyodhihirishwa katika Biblia na kuomba tu ndipo hatuwezi kuchoka kutenda mema, wala kuzimia njiani.

      Tena, inatupasa kumtafakari Yesu kwa sababu ndani yake Yeye "hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika."  Mtu awaye yote aliyepungukiwa na hekima anaelekezwa kumwomba Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei, na ahadi ni kwamba naye atapewa; walakini hekima hii inayohitajika inaweza kupatikana tu ndani ya Kristo.  Hekima ile isiyotoka kwake Kristo, na ambayo  matokeo yake hayamwongozi mtu huyo Kwake ni upumbavu mtupu; kwa  maana Mungu, aliye chimbuko la vitu vyote, ndiye mwanzilishi wa hekima;  ujinga wa kutomjua Mungu ni upumbavu ulio mbaya mno (Angalia Rum.1:21,22);  na hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika ndani yake Kristo; hata imekuwa kwamba mtu yule aliye na hekima ya ulimwengu huu peke yake, kwa kweli hajui kitu cho chote.  Na kwa kuwa mamlaka yote mbinguni na duniani amepewa Kristo, hii ndiyo maana mtume Paulo anamtangaza Kristo kuwa ndiye "nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.  1 Kor.1:24.

     Walakini kuna fungu moja ambalo kwa kifupi linatoa muhtasari wa mambo yote ambayo Kristo amekuwa kwa mwanadamu, nalo linatoa sababu inayojumuisha karibu mambo yote yahusuyo kumtafakari Yeye.  Fungu hilo ni hili:  "Bali kwa Yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi." 1 Kor.1:30. Sisi tu wajinga, waovu, na wapotevu; Kristo kwetu sisi ni hekima, haki, na ukombozi.  Ni upeo mpana ulioje!  Kutoka katika ujinga wetu na dhambi zetu na kuingia katika haki yake na ukombozi wake.  Tamaa au haja ya mwanadamu ya juu kuliko zote haiwezi kuvuka mipaka ya kile ambacho Kristo amefanywa kwetu sisi, wala vile ambavyo Yeye binafsi amekuwa kwetu sisi.  Hii ndiyo sababu ya kutosha kwa nini macho ya wote yamwangalie Yeye.