KUKUBALIKA NA MUNGU
Watu wengi husita-sita kuanza kumtumikia Bwana, kwasababu wanaogopa kwamba Mungu hatawakubali; na maelfu ya wale waliokwisha kuwa wafuasi wake Kristo kwa miaka mingi bado wanayo mashaka juu ya kukubalika kwao na Mungu. Kwa faida ya watu kama hao naandika, nami nisingependa kuwachanganya mawazo yao kwa kukisia, lakini nitajitahidi kuwapa ahadi za neno la Mungu zinazoeleweka.
"Hivi Bwana atanipokea mimi?" Najibu kwa kuuliza swali jingine: Je, hivi mtu atakipokea kile ambacho amekinunua? Ukienda dukani na kufanya ununuzi, je! utaweza kuzipokea bidhaa zile wanazokukabidhi? Bila shaka, utafanya hivyo; hakuna nafasi ya swali juu ya hilo. Ule ukweli kwamba ulizinunua bidhaa hizo, na kutoa fedha zako kuzilipia, huo ni ushahidi wa kutosha, sio tu kwamba wewe UNAZITAKA, bali kwamba UNAYO HAMU ya kuzipokea. Kama usingezitaka, usingezinunua. Zaidi ya hayo, kwa kadiri ulivyozilipia fedha nyingi, ndivyo kadiri ulivyo na hamu nyingi kuzipokea. Kama bei uliyolipa ilikuwa kubwa, nawe karibu ulijitoa mhanga maisha yako ili kukipata kitu hicho, basi, hapana swali ila ni kwamba utakipokea kile ulichokinunua mara tu utakapokabidhiwa. Wasiwasi wako mkubwa ni kwamba isije ikawa wakashindwa kukukabidhi kitu hicho.
Sasa basi, hebu na tukitumie kielelezo hiki rahisi na cha kawaida kuhusu shauri la mwenye dhambi anayemjia Kristo. Kwanza kabisa, Yeye ametununua sisi. "Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani." l Kor.6:l9,20.
Thamani iliyolipwa kwa ajili yetu sisi ilikuwa ni damu Yake Mwenyewe ---- uhai wake. Paulo aliwaambia wazee wale wa Efeso: "Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu Yake Mwenyewe." Mdo.20:28. "Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya Mwana-Kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo." l Petro l:l8,l9. Yeye "alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu." Gal.l:4.
Hakuwanunua watu wa tabaka fulani, bali ulimwengu mzima wa wenye dhambi. "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ULIMWENGU, hata akamtoa Mwanawe pekee." Yohana 3:l6. Yesu alisema, "Na chakula nita
kachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu." Yohana 6:5l. "Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu." "Bali Mungu aonyesha pendo lake Yeye Mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi." Rum. 5:6,8.
Thamani iliyolipwa ilipita upeo, kwa hiyo tunajua kwamba alikitamani sana kile alichokinunua. Alinuia kwa moyo wake wote kukipata. Angalia Wafilipi 2:6-8; Ebr.l2:2; Isa.53:ll.
"Lakini mimi sifai kitu." Hii ina maana kwamba wewe unajiona hustahili kununuliwa kwa thamani ile iliyolipwa, na kwa ajili hiyo unaogopa kuja isije ikawa Kristo akakataa kukipokea kile alichokinunua. Sasa huenda ukawa na hofu kiasi fulani kwa sababu hiyo endapo mapatano hayo hayakutiwa muhuri, na thamani ile ilikuwa haijalipwa bado. Kama angekataa kukupokea kwa sababu ya kwamba wewe hufai kwa thamani hiyo, asingekupoteza wewe tu, bali pia na thamani ile aliyolipa. Hata kama bidhaa zile ulizozilipia hazifai kwa thamani uliyotoa, wewe mwenyewe usingekuwa mpumbavu kiasi cha kuzitupilia mbali. Angalau ungepata faida kiasi fulani kwa bidhaa hizo kurudisha fedha zako ulizolipa kuliko kukosa vyote viwili.
Lakini, zaidi ya hayo, wewe huhusiki kabisa na suala la kufaa. Kristo alipokuwa hapa duniani akikitafuta kitu hicho cha kununua, "hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana Yeye Mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu." Yohana 2:25. Alikinunua kile alichotaka akiwa anaona kwa macho yake, naye alijua thamani yake halisi ya kile alichokinunua. Yeye hajakata tamaa hata kidogo unapokuja Kwake, naye anakuona kuwa hufai kitu. Haikupasi kuwa na wasiwasi juu ya suala hilo la kufaa kwako; ikiwa Yeye, aliye na ujuzi kamili wa hali yako ilivyo, aliridhika kufanya mapatano hayo, basi, wewe ungekuwa wa mwisho kulalamika.
Ukweli wa kushangaza kuliko wote ni kwamba alikununua wewe kwa sababu ile ile ya kwamba ulikuwa hufai kitu. Jicho lake lenye uzoefu liliona ndani yako uwezekano mkubwa, naye alikununua, si kwa vile ulivyo sasa kwa thamani yako, bali kwa kile ambacho angeweza kukufanyia wewe. Anasema: "Mimi, naam, mimi ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu Mwenyewe." Isa.43:25. Sisi hatuna haki yo yote, ndio maana alitununua, "Maana katika Yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika Yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka." Kol.2:9,l0. Mpango wote umeelezwa hapa:-
"Sisi sote ... tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda, hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo." Efe.2:3-l0.
Sisi tunapaswa "kuwa sifa ya utukufu wa neema Yake." Hilo lisingewezekana kama sisi kwa asili thamani yetu ingekuwa sawasawa na thamani ile aliyoilipa kwa ajili yetu. Katika hali hiyo usingekuwapo utukufu wo wote kwa tendo hilo. Asingeweza, katika zamani zinazokuja, kuudhihirisha wingi wa neema Yake. Lakini anapotuchukua sisi, tukiwa hatufai kitu, na hatimaye anatusimamisha pasipo makosa mbele ya kiti kile cha enzi, hapo ndipo itakuwa kwa utukufu Wake wa milele! Na wakati huo hapatakuwa na ye yote atakayejihesabu kuwa anafaa kwa ajili yake mwenyewe. Milele zote, jeshi lile la waliotakaswa litajiunga pamoja na kumwambia Kristo: "Wastahili Wewe ... kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu." "Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka." Ufu.5:9,l0,l2.
Hapana budi mashaka yote juu ya kukubalika na Mungu yangetulizwa. Lakini hivyo sivyo ilivyo. Moyo huu mbovu wa kutokuamini bado unaleta fikira za mashaka. "Nasadiki hayo yote, lakini ----." Hapo, simama papo hapo; kama ungeamini usingeweza kusema "lakini". Watu wanapoongeza "lakini" kwa usemi ule wanaousadiki, basi, wanamaanisha hasa kwamba, "Nasadiki, lakini sisadiki." Lakini wewe unaendelea kusema: "Huenda unasema kweli, lakini, basi, nisikilize mpaka mwisho. Nililotaka kusema ni hili, Nasadiki usemi uliomo katika Maandiko uliyoyanukuu, lakini Biblia iyo hiyo inasema kwamba kama sisi ni wana wa Mungu, basi, tutakuwa na ushuhuda wa Roho, na ushuhuda huo utakuwa ndani yetu wenyewe; mimi sijisikii ndani yangu kwamba ninao ushuhuda wo wote kama huo, kwa hiyo mimi SIWEZI kuamini ya kuwa mimi ni wake Kristo. Naliamini neno lake, ila sina ushuhuda huo." Naelewa utata wako; hebu nione kama hauwezi kuondolewa.
Kwa suala lile la kuwa wake Kristo, wewe mwenyewe unaweza kulimaliza. Umekwisha kuona alivyojitoa nafsi yake kwa ajili yako. Sasa swali lenyewe ni hili, Je, umejitoa nafsi yako mwenyewe Kwake? Kama ni hivyo, unaweza kuwa na hakika kwamba anakukubali. Kama wewe si Wake, basi, ni kwa sababu tu wewe umekataa kumkabidhi kile alichokinunua. Unamrubuni. Yeye anasema, "Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi." Rum.l0:2l. Anakusihi umkabidhi kile alichokinunua na kukilipia, lakini ambacho wewe unakataa kumkabidhi, huku ukimlaumu kwamba hataki kukupokea. Lakini kama kwa moyo wote umejikabidhi Kwake kuwa mwana wake, basi, uwe na hakika kuwa amekupokea.
Sasa kuhusu kusadiki kwako maneno Yake, lakini huku ukiwa na mashaka kama amekupokea, kwa sababu husikii ushuhuda huo moyoni mwako, mimi bado nasisitiza kwamba wewe husadiki. Kama ungesadiki, basi, ungekuwa na ushuhuda huo. Sikiliza neno Lake: "Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake." l Yohana 5:l0. Kumwamini Mwana ni kule kuliamini neno lake na habari zile zinazomhusu Yeye.
Na "YEYE AMWAMINIYE MWANA WA MUNGU ANAO HUO USHUHUDA NDANI YAKE." Huwezi kuwa na ushuhuda mpaka kwanza uamini; na mara tu unapoamini, unao huo ushuhuda. Inakuwaje? Kwa sababu IMANI YAKO KATIKA NENO LA MUNGU NDIYO USHUHUDA WENYEWE. Ni Mungu anayesema hivyo:
"Basi IMANI NI KUWA NA HAKIKA ya mambo yatarajiwayo, ni BAYANA ya mambo yasiyoonekana." Ebr.ll:l.
Kama ungeweza kumsikia Mungu akisema kwa sauti inayosikika akikuambia kwamba wewe ni mwana Wake, ungeyafikiria maneno hayo kuwa ni ushuhuda wa kutosha. Basi, Mungu anaposema katika neno lake, ni sawasawa kana kwamba anasema kwa sauti yake inayosikika; na imani yako ni ushuhuda kwamba unasikia na kuamini.
Jambo hili ni la muhimu sana kiasi kwamba linastahili kulitafakari kwa makini. Hebu na tuendelee kidogo zaidi kusoma habari zake. Kwanza, tunasoma kwamba sisi tu"mekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu." Gal.3:26. Huu ni uthibitisho dhahiri juu ya kile nilichosema kuhusu kutokuamini ushuhuda huo. Imani yetu ndiyo inayotufanya kuwa wana wa Mungu. Lakini, je, tunaipataje imani hii? ---- "Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo." Rum.l0:l7. Lakini, je! tutaipataje imani hii katika neno la Mungu? ---- Amini tu kuwa Mungu hawezi kusema uongo. Usingeweza hata kidogo kumwita Mungu kuwa ni mwongo mbele za macho Yake; lakini hivyo ndivyo unavyofanya kama huliamini neno Lake. Yote yakupasayo kufanya ili kuamini ni KUAMINI. "Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile nelo la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika." Rum.l0:8-ll.
Maneno yote haya yanapatana na habari aliyopewa Paulo: "Roho Mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye." Rum.8:l6,l7. Roho huyu anayeshuhudia pamoja na roho zetu ni yule Msaidizi [Mfariji] aliyeahidiwa na Kristo. Yohana l4:l6. Nasi tunajua kwamba ushuhuda Wake ni wa kweli, maana Yeye ni "Roho wa Kweli." Sasa, je! anatoaje ushuhuda Wake? ---- Kwa kutukumbusha neno lililoandikwa. Yeye ndiye aliyeyavuvia maneno hayo (l Kor.2:l3; 2 Petro l:2l), na, kwa ajili hiyo, anapotukumbusha maneno hayo, ni sawasawa kana kwamba alikuwa anayatamka maneno hayo moja kwa moja kwetu. anatukumbusha habari, ambayo sehemu yake tumekwisha kuinukuu; tunajua kwamba habari hiyo ni ya kweli, maana Mungu hawezi kusema uongo; kwa hiyo tunamwamuru Shetani kwenda zake pamoja na ushuhuda wake wa uongo juu ya Mungu, nasi tunaiamini habari hiyo, basi, tunajua kwamba sisi ni watoto wa Mungu, na tunalia, "Aba, Baba." Na hapo ndipo ukweli huu mtukufu unapong'aa kwa ukamilifu rohoni mwetu. Kuyakariri maneno hayo huyafanya yawe kweli kwetu sisi. Yeye ndiye BABA YETU; sisi tu watoto Wake. Ni furaha ilioje wazo hilo linatuletea! Hivyo tunaona kwamba ushuhuda uliomo ndani yetu sisi wenyewe sio kule kuchomwa mara moja ama kujisikia moyoni mwetu. Mungu hatutaki sisi kutegemea kitu kisichoaminika kabisa kama kujisikia moyoni mwetu. Anayeutegemea moyo wake ni mpumbavu,yasema Maandiko. Lakini ushuhuda ule tunaopaswa kuutegemea ni lile neno la Mungu lisilobadilika, na ushuhuda huo tunaweza kuupata kwa njia ya Roho, katika mioyo yetu wenyewe. "Mungu ashukuriwe kwa sababu ya kipawa chake."
Ushuhuda huo hautupi ruhusa ya kulegeza juhudi zetu na kuketi chini tukiwa tumetosheka, kana kwamba tulikuwa tumeupata ukamilifu. Yatupasa kukumbuka kwamba Kristo anatukubali si kwa ajili yetu wenyewe, bali kwa ajili Yake Mwenyewe; si kwa sababu tumekuwa wakamilifu, bali kwamba ndani Yake tuendelee kuuchuchumilia ukamilifu huo. Anatubariki, si kwa sababu tumekuwa wema sana kiasi cha kustahili baraka hiyo, bali ili kwa njia ya nguvu ya baraka hiyo sisi tupate kugeukia mbali na maovu yetu. Mdo.3:26. Kwa kila mmoja anayemwamini Kristo, uwezo ---- haki ama upendeleo ---- unatolewa ili tupate kuwa watoto wa Mungu. Yohana l:l2, pambizo. Ni kwa njia ya "ahadi kubwa mno, za thamani" za Mungu kupitia kwake Kristo kwamba sisi tunapata "kuwa washirika wa tabia ya Uungu." 2 Petro l:4.
Hebu na tutafakari kwa kifupi matumizi ya baadhi ya Maandiko haya katika maisha yetu.